Sunday, October 23, 2016

MALKIA WA SHINDANO LA UREMBO KWA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI ‘ALBINO’ KENYA APATIKANA


Akina dada walioshiriki katika mashindano ya urembo kwa watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi ama Albinos jijini Nairobi, Kenya. Tarehe 21 Oktoba 2016.
Mamia walijitokeza kushuhudia maonyesho ya urembo ya Mr na Ms Albino nchini Kenya. Kila siku Albino wanakabiliwa na hatari ya kuuawa na viungo vyao vya mwili kuuzwa kutokana na imani za kishirikina Afrika mashariki na Afrika kusini.Chanzo-BBC SWAHILI
Malkia mpya! Louise Lihanda, aliyeshinda taji la urembo kwa akina dada atembea jukwani akiwa amevalia vazi la kupendeza lililotengenezwa kwa kutumia puto. Loiuse ambaye ni mwanafunzi, amekuwa mwanamke wa kwanza kushinda taji hilo, katika mashindano yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya tarehe 21 Oktoba 2016
Wanaume walioshiriki katika mashindano hayo wasimama  jukwaani. walishiriki katika mashindano ya urembo kwa watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi ama Albinos jijini Nairobi, Kenya. Tarehe 21 Oktoba 2016.
Mfalme! Jairus Ongetta, ambaye amekabidhiwa taji ya uanamitindo bora kwa wanaume akiwa jukwaani na mavazi ya kupendeza.
Erick Thomas, awaongoza wanamitindo wenzake kwenye jukwaa wakati wa mashindano ya urembo kwa watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi. Lengo lake ni kuhakikisha kwamba watu walio na ulemavu huo wamejivunia ngozi yao.
Msichana huyu aliduwazwa na maonyesho hayo! Yeye ni miongoni mwa watu ambao kila siku wanakabiliwa na hatari ya kuuawa kutokana na imani za kishirikina Afrika mashariki na Afrika kusini.
Miraba minne! John Ngatia, ambaye pia huwa anasakata densi, avalia sare ya mapigano ya ndondi katika maonyesho hayo, jijini Nairobi Kenya tarehe 21 Oktoba 2016
Majaji walikuwa macho! Waliongozwa na mwanamitindo wa kimataifa Deliah Ipupa (katikati) tarehe 21Oktoba 2016.
Naomi Wafula, ajitokeza jukwaani akiwa amevalia vazi lililotengenezwa kwa sahani za plastiki katika mashindano ya urembo yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya tarehe 21 Oktoba 2016
Mamia walihudhuria maonyesho hayo kuonyesha umoja wao na watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi katika mgahawa wa Carnivore jijini Nairobi Kenya, tarehe 21, Oktoba 2016
 
 Amina Makokha ajitokeza jukwaani akiwa amevalia sare ya mchezo wa raga katika mashindano ya urembo yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya tarehe 21 Oktoba 2016


Kutoka kulia, naibu rais wa Kenya William Ruto, Mbunge Isaack Mwaura na mkurugenzi mkuu wa bodi ya filamu nchini Kenya Ezekiel Mutua pia walikuwemo.

MANGULA AFURAHISHWA 100 KUFUKUZWA UANACHAMA WA CCM MWANZA

Mzee Philip Mangula
Na Bashir Nkoromo, Mkuranga
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula ameelezea kufurahishwa kwake kufukuzwa kwa wanachama 100 mkoani Mwanza kwa kubainika kukisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

"Haiwezekani, unajiita mwanachama, halafu badala ya kujitolea kwa nguvu zako zote chama kishinde vita ya kushika dola, wewe unakisaliti,  hapo unakuwa si mwanachama bali jeshi la kukodiwa",  Mangula alisema, hayo jana, wakati akizungumza na Vijana wanaosoma na waliohitimu vyuo vikuu 20, ambao wameweka kambi ya kufyatua matofali kwa ajli ya ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu katika shule ya Sekondari Nasabagani, Mkuranga mkoa wa Pwani.

 "Taarifa ya Chama kuwafukuza uanachama wale 100 kule Mwanza imenifurahisha sana, ni matumaini yangu kwamba hatua kama hizi zitaendelea kuchukuliwa  kila mahala nchini kote kwa waliokisaliti chama. hivi ni mchezaji gani anayempiga ngwara mchezaji wa timu yake wakati wa mechi ya kutafuta ubingwa halafu akaachwa kuendelea kuwa katika timu?" Mangula alisema na kuhoji kwa mshangao.

Mangua alisema, wakati mikoa itaendelea kuchukua hatua, lakini pia kwa ngazi ya taifa hatua dhidi ya waliokisaliti chama zitaendelea kuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuwatupilia mbali watakaojaribu kuomba nafasi za uongozi wakati wa uchaguzi wa Chama mwakani, huku wakiwa wameshabainika kuwa walikisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu ulipita.

Mangula aliwataka vijana nchini kote hasa wasomi, kuepuka kutumiwa vibaya na wanachama watakaokuwa wanasaka uongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani, kwa kuwa kijana yeyote atakayekubali kutumiwa vibaya atakuwa amekisaliti na kuchangia kunyong'onyesha nguvu na uhai wa Chama.

"Hili la kutumiwa vibaya hasa ninyi vijana, nawaasa sana kuepuka nalo, jambo hili ni baya sana, na si kwa Chama tu lakini hata kwa wewe uliyekubali kutumika, maana utatumiwa kama ngazi, halafu akishapita hatakuwa na manufaa kwako na hata kwa taifa maana atakuwa mvurugaji tu, badala ya kushiriki kuleta maendeleo ya chama na taifa", Alisisitiza mangula.

Alisema, vijana hao 53 waliojitolewa kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi huo wa mabweni na nyumba za walimu, wameonyesha moyo mkubwa wa uzalendo kwa nchi yao, na kwamba huo ndiyo uzalendo wa kweli unaopaswa kuonyeshwa na kila mwananchi hasa viongozi katika ngazi mbalimbali.

Mangula alisema, vijana hao wameoyesha mwamko ule uliokuwa umejengwa na kuwepo wakati wa Baba wa taifa Mwalimu Nyerere, ambao katika miaka ya hivi karibuni hasa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi umetoweka kwa watu kuanza kujinasibu kwa majina ya vyama vyao vya siasa badala ya kuonyesha uzalendo kwa kuisaidia jamii kwa za kujitoea.

Alisema, umefikia wakati sasa kipimo cha kwanza kwa yeyote kupata uongozi iwe ni kutazamwa kama kweli ni mzalendo ambaye yupo mstari wa mbele kufanya kazi za kujitolea katika jamii, na siyo kutazama uwezo wake wa kuzungumza na kumwaga hotuba nzuri majukwaani.

"Sifa za mtu kupewa uongozi isiwe ukasuku wa kutoa talalila za hotuba nzuri za kisiasa majukwaani, kwanza atazwamwe kama amekuwa akitoa mchango gani kwa jamii kwa kufanya kazi za kujitolea katika kusukuma maendeleo ya taifa mbele kama ilivyokuwa wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, hongereni sana vijana kwa kuonyesha moyo wa kfufua uzalendo.", alisema  Mangula.

Mapema, Katibu wa Kambi ya vijana hao, Daniel Sarungi, alisema, tangu walipoanza kambi hiyo, na kuanza kufyatua matofali Septemba 29, 2016, wameshafywatua matofali zaidi ya 30,000, kati ya lengo lao la matofali 45,000, ambalo watahakikisha wamelifikia kesho Oktoba 24, 2016.

Alisema, vijana hao wamejikusanya kutoka vyuo vikuu 20, vutatu vikiwa ni vya nchi za nje, na wamekuwa wakishirikiana vizuri, tangu kusomba mchanga na kufyatua matofali, kujipikia chakula, kufundisha wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule hiyo, kutoa huduma ya afya, kushiriki michezo mbalimbali na kufanya semina na mijadala ya kukuza uwezo wa kuleta maendeleo katika jamii.

Sarungi alisema, vijana hao ambao baadhi wameshahitimu masomo na wengine bado wanasoma katika taaluma mbalimbali wameamua kujitolea kusaidia ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu, baada ya kuguswa na adha ya kulala chini wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita katika shule hiyo huku walimu na wakiwa hawana nyumba za kutosha kuishi.

Wakati wanafunzi waliopo sasa wanalala chini katika chumba cha maabara, nyumba moja yeneye nyumba vitatu inatumiwa na walimu saba kuishi katika nyumba hiyo, haliambayo hairidhishi.


Mapema, Mangula alishiriki kufyatua matofali na baadaye kusema kwamba aliamua kwenda kuwaunga mkono vijana hao baada ya kusikia taarifa zao kwenye vyombo vya habari hatua yao ya kuamua kujitolea kusaidia shule hiyo baada ya kuhamasishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga ambaye siyo tu amekuwa akiratibu bali amekuwa pia ashiriki katika ufyatuaji huo wa matofali.

WAZIRI MAKAMBA AKATAZA UCHEPUSHAJI WA VYANZA VYA MAJI


Na Lulu Mussa-Songwe

Wakazi wa Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe wamehamasishwa kutunza Vyanzo vya Maji kwakuwa Maji hayana mmadala wa kitu chochote. Waziri wa Nchi mwenye dhamana ya Usimamizi wa Masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba ameyasema hayo leo katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua mazingira nchini.

Akiwa katika Kijiji cha Ibungu Wilayani Ileje, Waziri Makamba alishuhudia uliochepushwaji wa Mto Kalembo kwa manufaa ya baadhi ya mtu/watu, na haikuweza kufahamika mara moja muhusika. Aidha Waziri Makamba amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ileje Bw. Joseph Modest Mkude kuhakisha wanambaini mtu/watu hao na kuwafisha katika vyombo vya Sheria.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Ileje ilisema kwamba kumekuwa na uvamizi katika Vyanzo vya Maji na Serikikali imeendelea na juhudi za kuwaondoa kwa kuwapatia maeneo mengine ila baadhi ya wananchi hao wamekuwa wakikaidi. Hali hiyo haikumfurahisha Waziri Makamba na kuagizia kutumika mamlaka ya Dola. “Hatuwezi kuruhusu watu kuharibu Vyanzo vya Maji na kuwabembeleza watoke” Makamba alilisitiza.

Waziri Makamba amesema ni muhimu watu kutii Sheria na Mamlaka zilizopo, ameagiza wakazi hao kupewa wiki mbili tu na baada ya hapo waondolewe kwa nguvu kwani tayari maeneo mbadala kwa makazi yao yalisha ainishwa. Pia Waziri Makamba ameahidi kutoa muongozo wa Sheria ndogondogo za Mazingira za Vijiji na Vitongoji ili zitumike kama nyenzo za hifadhi ya Mazingira Nchini.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba alitembelea Kijiji cha Lubanda, Kata ya Lubanda na kufanya Mkutano wa hadhara na wananchi na kuwasisitizia, kutokokata miti ovyo, kutochoma misitu na kuepuka uchepushaji wa Vyanzo vya Maji ikiwemo mito na Mabonde.

Pia Waziri Makamba aliwashauri wakazi wa Lubanda kulima kilimo cha Matuta ama makinga maji ili kuepuka mmomonyoko wa udongo katika miinuko. Aidha Waziri Makamba ameunga mkono jitahada za wananchi wa Kata hiyo za ujenzi wa Kituo cha afya kwa kuchangia bati Ishirini na nane (28). Waziri Makamba anaendelea na ziara yake na leo amewasili katika Mkoa wa Rukwa.

Uharibifu wa Mazingira unaofanywa na binadamu, pichani ni Mto Kalembo uliopo katika Kijiji cha Ibungu Wilayani Ileje uliochepushwa kwa manufaa ya baadhi ya mtu/watu, haikuweza kufahamika mara moja muhusika. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Ileje Bw. Joseph Modest Mkude kutafuta wahusika na kuwafikishwa kwenye Vyombo vya dola.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akifafanua jambo kwa wananchi mara baada ya kuwapa fursa ya kuuliza maswali katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Lubada Wilayani Ileje. Kushoto ni Bw. Stanford Kibona aliyeuliza swali.

VICHWA VYA HABARI YA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI OKTOBA 23,2016