Wednesday, August 20, 2014

ZSTC na jitihada za kuinua wakulima wa karafuu Zanzibar

 SHIRIKA la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) ni Shirika la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar lililoanzishwa mwaka 1968 kwa madhumuni ya kununua na kuuza mazao ya wakulima kama vile karafuu, mbata, makonyo, pilipili hoho, makombe na mwani.

Shirika hilo tokea wakati huo wa miaka ya sitini limekuwa likitimiza wajibu huo na majukumu mengine  iliyopewa na Serikali kwa ufanisi na kwa uwazi ili kutoa huduma nzuri kwa wakulima na wauzaji wa mazao hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yaliwapatia wananchi wa visiwani faida kubwa.
Visiwa vya Zanzibar ni visiwa vinavyosifika kwa uzalishaji wa zao la karafuu bora ambalo pia katika miaka mingi ya nyuma, vilitajika kwa uzalishaji wa kiwango cha juu cha karafuu duniani.


Wananchi wengi wakati huo walikuwa wakizithamini mno karafuu kutokana na umuhimu wake wa kuwapatia kipato, lakini, pia kama zao tegemezi la uchumi wa Zanzibar katika kupata fedha za kigeni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.


Akizungumza na Zanzibar Leo katika mahojiano maalum ya mafanikio ya Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), Naibu Mkurugenzi Muendeshaji wa Shirika hilo, Jongo Suleiman Jongo, alisema, 
ZSTC imepitia katika hatua mbalimbali za mafanikio na changamoto tokea lilipoanzishwa mwaka 1968.

Alisema, ZSTC ilikuwa kila kitu katika uagizaji wa bidhaa za biashara na Shirika hilo tangu wakati huo wa miaka ya sitini, lilikuwa likitimiza wajibu huo na majukumu mengine  iliyopewa na Serikali kwa ufanisi na kwa uwazi ili kutoa huduma nzuri kwa wakulima na wauzaji wa mazao hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yaliwapatia wananchi wa Zanzibar faida kubwa.

Alisema, katika miaka ya 1980-90, Shirika la ZSTC pamoja na kuwa lilikua likiendeleza majukumu hayo, lakini, pia Serikali kwa nia safi ilitoa nafasi kwa wananchi wake wenye uwezo wa kulima na kusafirisha mazao ya mbata, pilipili hoho, makombe na mwani kufanya hivyo ili kuongezea kipato chao. 

Ni kipindi ambacho Zanzibar ilishuhudia mageuzi makubwa ya kibiashara chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, ambapo ZSTC ilipunguziwa baadhi ya majukumu  na kukabidhiwa kwa sekta binafsi na sababu kubwa ilikuwa ni Serikali kujitoa katika kufanya biashara na kuwaachia wananchi wake.
"Hapa ndipo tuliposhuhudia mazao kama vile ya mbata, makomwe, pilipili hoho na mwani zikiachwa na ZSTC na kukabidhiwa sekta binafsi", alisema.


Hata hivyo, alisema, sekta hiyo haikufanya vizuri kuendeleza biashara hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya bei walizoziweka ndani na nje ya soko kutokwenda sawia kibiashara.

Alisema, hilo ni tofauti kidogo na upande wa serikali ambayo wakati mwengine hulazimika kujipiga kifua pale soko linapoanguka na kujibebesha dhamana ya kubakia na bei hata kama inakwenda kwa hasara katika kipindi hicho.

Naibu huyo, alisema, kazi za ZSTC wakati huo zilikuwa ni kununua mazao ya wakulima pamoja na kuuza nje mazao hayo na kwamba jitihada zilizofanywa wakati huo zilizaa matunda na kuchangia sehemu kubwa ya mapato ya serikali.

Alisema, katika miaka hiyo, zao la karafuu lilikuwa ndiyo tegemeo kubwa la pato la kiuchumi katika visiwa vya Zanzibar na kuiwezesha kuendesha mipango yake ya kiuchumi na kijamii bila ya kuyumba. Hali hiyo ilitokana na ukubwa wa soko la dunia na ubora wa kipekee wa karafuu za Zanzibar katika soko hilo. 

Hata hivyo, alisema, kwenye miaka ya 1990, hali ya soko haikuwa nzuri sambamba na kushuka kwa bei na kuongezeka kwa nchi zinazozalisha karafuu duniani na hivyo kuleta ushindani wa kibiashara.
Kushuka kwa bei katika soko la dunia kulipelekea kushuka kwa ari ya  uzalishaji kwa wakulima na kupelekea visiwa vya Zanzibar navyo kupoteza muelekeo wa zao hili. Zao hili lilipoteza hadhi yake ya kuwa zao la uchumi wa nchi. 

Alisema, wakulima wengi waliacha kulima zao la karafuu na badala yake walijihughulisha na mazao mengine ukiwemo ukulima wa mwani ambapo wakati huo ulionekana kama ungelikuwa mbadala wa zao la karafuu. 

Alisema, pamoja na kuyumba kwa soko la dunia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliendelea kununua karafuu kutoka kwa wakulima, ingawa si kwa bei ya kiwango cha juu. Serikali ililazimika wakati mwengine kufidia gharama za bei katika kuona mkulima ambaye ni mwananchi anaendelea kujenga imani na kulithamini zao la karafuu.


Hata hivyo, alisema, pamoja na Shirika la ZSTC kuwa lilikua likiendeleza majukumu hayo, katika miaka ya 1990 -2010, hali haikuwa nzuri kutokana na kushuka kwa zao la karafuu huku wakulima nao wakiacha kuliendelea zao hilo na kujishughulia na mambo mengine ya kimaisha.


MABADILIKO YA SHIRIKA 2010/11

Mara baada ya kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Saba chini ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein, mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ya ZSTC na uzalishaji wa zao la karafuu yalifanyika.
Dk. Shein alianzisha mkakati wa miaka 10 wa maendeleo ya zao la karafuu wenye lengo la kulifufua upya zao hilo kwa kuongeza uzalishaji na uzaji ambapo utekelezaji wa mkakati huo (2011/2021) ulianza kwa kulijenga upya Shirika la ZSTC.
Mabadiliko hayo yametiwa nguvu na sheria namba 11 ya mwaka 2011 ambapo yameliwezesha Shirika la ZSTC kuwa imara kimkakati juu ya kubadilisha mtazamo wa wakulima juu ya zao la karafuu, utekelezaji wa sera ya karafuu na limekuwa imara zaidi katika ushindani wa soko la ndani na nje.
Mwanasheria wa ZSTC, Ali Hilal Vuai, anasema, moja ya jukumu ambalo shirika hilo imepewa na serikali ni kuhamasisha uzalishaji wa zao la karafuu, kuwasaidia wakulima katika hali nzima ya uimarishaji wa zao hilo.
Hivyo, alisema,  shirika  limekuwa likitoa mikopo ya fedha  kwa wakulima wa karafuu Unguja na Pembe, lengo ni kuwasaidia wakulima kumudu gharama za awali za uchumaji na baadaye kuzirudisha fedha hizo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mwengine na kuendeleza kilimo cha karafuu.
Hata hivyo, alisema, baadhi ya wakulima wamekuwa hawarejeshi mikopo hiyo na wale wanaorudisha, hushindwa kufuata wakati na hivyo kupelekea usumbufu kwa ajili maandalizi ya msimu mwengine.
“Kimsingi huu hasa si mkopo,ni msaada kwa vile hauna riba na mkulima hurejesha kile kile alichokikopa ZSTC”, alisema.
“Shirika limekuwa likitoa fedha nyingi kuwakopesha wakulima, lengo hapa ni kufanya shughuli endelevu za awali za karafuu kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa ujumla”.
Aidha Serikali imeongeza bei ya karafuu ambapo mkulima analipwa 80% ya bei inayouzwa nje ambapo kutokana na bei hiyo wananchi sasa wamerejea katika kulirudishia heshima zao hilo.
Hali hiyo ilikwenda sambamba na upungufu wa karafuu katika soko la dunia na hivyo kutumiwa vizuri na Serikali chini ya ZSTC kulistawisha upya zao kwa kuweka bei nzuri kwa wakulima.
Tokeo hapo chini ya Dk.Shein, hali ya bei ya karafuu haijashuka chini ya shilingi 10,000 kwa mkulima, ikiwa ni asilimia 80% ya bei inayouzwa katika soko la dunia pamoja na mazingira mazuri ya kununua zao hilo yanayowavutia wakulima kuuza karafuu zao kupitia ZSTC na kuachana na magendo yaliyokuwa yameshamiri katika kipindi kirefu.
Naibu Mkurugenzi huyo, anasema, sera ya sasa ya karafuu  imebadilika tofauti na miaka ya nyuma ambapo hivi sasa  inaangalia kumnufaisha mkulima na Taifa kwa ujumla.



MTAZAMO WA SASA WA ZSTC

Mtazamo wa sasa wa hali ya kibiashara ya nje ni ZSTC kuelekea katika kutafuta mazao zaidi ya karafuu pamoja na kuzalisha bidhaa zitokanazo na zao hilo la karafuu (Packages).
ZSTC kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo inaendelea na mikakati ya kuimarisha zao la karafuu ikiwemo juhudi za kuotesha miche mingi hadi kufikia milioni moja kwa mwaka.
Alisema, ZSTC chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mwendeshaji Bi Mwanahija Almas Ali, imekuwa yenye malengo yanayotekelezeka, malengo hayo ni pamoja na mabadiliko ya utendaji wa shirika hilo.
"ZSTC sasa tupo vizuri hatukopi fedha kutoka sehemu yoyote, serikali ina pato lake na hayo ni mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kwa Shirika", alisema 
"ZSTC ilikuwa ikitumia si zaidi ya shilingi bilioni tano kununulia karafuu, lakini, sasa tunatumia zaidi ya bilioni 60, ni maendeleo makubwa".
"Tumekuwa tukichangia pato la taifa na kutoa ajira kwa sehemu kubwa katika zao la karafuu".
"Wananchi wamejitahidi  katika upandaji wa mikarafuu kufuatia mabadiliko ya mtazamo chanya wa ZSTC", Naibu huyo alieleza kiujumla juu ya mafanikio mengi ya shirika hilo la serikali.
Pamoja na kumiliki majengo ya kibiashara, maghala na kujenga vituo vya manunuzi vyenye hadhi ambapo huduma zote muhimu zinapatikana ikiwemo ulinzi, ZSTC inakusudia kuanzisha vyanzo vyengine zaidi vya kibiashra ili kujijengea uwezo zaidi. 
MAGEUZI YA KIUTENDAJI
ZSTC inaendelea na Mpango wa Mageuzi ya Kiutendaji ambapo ilisimamia mambo kadhaa ya kiufanisi ya shirika hilo ikiwemo kupunguza wafanyakazi na kuwalipa stahiki zao sambamba na uimarishaji wa vituo vya ununuzi wa karafuu.
Aidha imejizatiti katika uimarishaji wa masoko ya karafuu katika soko la ndani, soko la utalii, masoko ya kikanda na kimataifa kwa nia ya kuhakikisha karafuu ya Zanzibar haikosi soko.

MTAZAMO WA BAADAYE

Malengo ya baadae ya ZSTC ni kuendelea kuliimarisha zao la karafuu na kuhakikisha inachukuwa nafasi ya kwanza katika kuchangia pato la Taifa na fedha za kigeni ambapo kwa sasa inashikiliwa na sekta ya utalii.

CHANGAMOTO

Miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili ZSTC ni utaratibu wa ulipaji wa malipo  ya fedha taslimu kwenye vituo kutokana na wakulima wengi kutotumia huduma za Benki.
Baadhi ya Wakulima kutotumia majamvi katika uanikaji wa karafuu pamoja na elimu ya njia sahihi ya uanikaji kwenye najamvi kutolewa ambapo hali hiyo inaweza kuhatarisha ubora wa karafuu za Zanzibar.
Baadhi ya wakulima kutokufuata utaratibu unatumika vituoni ikiwemo kutofuata muda muafaka wa uuzaji wa karafuu kwenye vituo vya manunuzi. 
Baadha ya wakulima wagumu kulipa madeni ya fedha wanazokopeshwa ZSTC kwa ajili ya uchumaji wa zao hilo la karafuu apambo kufanya hivyo kunapunguza nguvu za Shirika kutoa huduma za kuliimarisha zao hilo.
Kwa mujibu wa Mwanasheria huyo, changamoto nyengine kubwa ya ZSTC sasa kujipanga kuhakikisha mikopo hiyo inarudishwa katika hali yote yote  ikiwa pamoja na kufikiria utaratibu kuziuza  mali zilizowekwa dhamana kwa ajili ya mikopo.
Hivyo, aliwataka wakulima wa karafuu kuitumia mikopo kwa manufaa zaidi kwa kulipa kwa wakati uliowekwa ili kuwawezesha wakulima wengine nao kufaidika na mikopo hiyo.  

No comments: