Monday, August 31, 2015

PROFESA SAID AHMED MUHAMMED APOKEA NAKALA YA ‘PAKA WA BINTI HATIBU’

- Naye akabidhi nakala ya kitabu chake kipya kiitwacho; ‘KAMWE SI MBALI TENA’
 Profesa Said Ahmed Muhammed (aliyevaa miwani) akimpa nasaha mwandishi wa ‘Paka wa Binti Hatibu’ Bwana Yussuf Shoka Hamad.
 Profesa Said Ahmed Muhammed akipokea nakala ya ‘Paka wa Binti Hatibu’ kutoka kwa mwandishi wa kitabu hicho Bwana Yussuf Shoka Hamad.
  Profesa Said Ahmed akimkabidhi Bwana Yussuf Shoka Hamad nakala ya kitabu chake kipya kiitwacho; ‘Kamwe si Mbali Tena’ nyumbani kwake Limbani, Wete.


Profesa Said Ahmed na Bwana Yussuf Shoka wakionesha nakala za vitabu vyao walivyoandika na kukabidhiana leo hii.

Na: Salum Msellem
Mwandishi mashuhuri wa kazi za fasihi ya Kiswahili nchini na mwalimu mzoefu katika midani ya lugha na fasihi ya Kiswahili, Profesa Said Ahmed Muhammed amepokea nakala adhimu ya kitabu cha ‘Paka wa Binti Hatibu’ kutoka kwa mwandishi chipukizi wa tasnia hiyo Bwana Yussuf Shoka Hamad .
Tukio hilo lilifanyika leo huko nyumbani kwa Profesa Said, Limbani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati mwandishi huyo chipukizi alipomtembelea mwandishi huyo nguli wa Afrika Mashariki na kujadili mambo mbali mbali yahususyo uandishi na taaluma.
Katika makabidhiano hayo, Profesa Said alimshukuru sana Bwana Yussuf  Shoka kwa juhudi zake na ujasiri alioonyesha wa kuandika kitabu hicho ambacho kwa sasa kimejinyakulia umaarufu mkubwa katika ulimwengu wa Kiswahili duniani.

Akizungumza kuhusu mapokezi ya kazi yake hiyo Bwana Yussuf alisema, kwa hakika kitabu kimeuza na kupokelewa kwa kasi kubwa ambapo kwa sasa ameuza nakala nyingi za kitabu hicho na bado kuna mahitaji makubwa ya kazi hiyo hasa hasa visiwani Zanzibar.

‘Kwa hakika nimeshangazwa sana na jinsi jamii ilivyompokea Paka wa Binti Hatibu. Juzi juzi tu nilikuja na nakala hamsini (50) lakini kwa muda usiozidi siku tatu niliuza  nakala hizo zote. Na hadi sasa kuna orodha ndefu ya wasomaji wanataka kitabu hicho. Kwa kweli nashukuru sana na nimeemewa sana na mapokezi ya kazi yangu hii!’ Alisema Bwana Yussuf.

Akizungumza kuhusu washabiki wake wakubwa na wasomaji wa kazi yake hiyo Bwana Yussuf alisema;
‘Nimefurahishwa sana kuona jinsi gani jamii yetu inathamini kazi za waandishi wazawa. Tena hata kwa wasomaji wasiokuwa wa fani ya fasihi. Kwa mfano, nimeuza nusu ya nakala zote kwa wafanyakazi wa PBZ, Pemba na zilziobaki kwa wanafunzi na walimu wa Chuo kikuu Huria cha Tanzania, tawi la Pemba. Kwa kweli nashukuru sana kwa kuungwa mkono kiasi hiki!’

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kitabu hicho, Profesa Said alimnasihi mwandishi huyo chipukizi nchini kutovunjika moyo na changamoto nyingi zinazomkabili kwa sasa na kumtaka aendelee kuandika na kuielemisha jamii kwa kadiri ya vile anavyoimulika na kuiakisi kwa minajili ya kuleta mabadiliko na maendeleo katika jamii ya Tanzania, Afrika Mashariki na Ulimwengu kwa ujumla.

Profesa pia alimtaka mwandishi huyo anayejulikana zaidi kwa kazi yake ya ‘Paka wa Binti Hatibu’ kuongeza kasi ya uandishi na kumtaka aisivunjike moyo hata kidogo katika kukabiliana na shida zilizopo katika tasnia ya uandishi hasa hasa za uchapishaji.
‘Nasaha zangu ni kukutaka tu uendelee kuandika kwa kasi hiyo hiyo. Usivunjike moyo kwani naona unaenda na kasi nzuri kwa sasa.’
Mwandishi Yussuf Shoka Hamad hadi sasa ameshakamilisha kazi yake ya ‘Paka wa Binti Hatibu’ na sasa anatarajia kuchapisha vitabu vyengine vitano mwaka huu pindipo kazi hizo zitachapishwa kwa wakati unaofaa.
‘Kwa kweli kuna msoyoyo mkubwa katika kuchapisha kazi siku hizi. Mchapishaji anaweza kuchukua mua mrefu sana kukupatia majibu ya muswada wako na hata kuuchapisha. Hii inarudisha nyuma kidogo kwa kweli’ Alisema Bwana Yussuf Shoka kumwambia Profesa Said.
Kuhusiana na kadhia hiyo, Profesa alimtaka Bwana Yussuf kujaribu kuwasiliana na wachapishaji wengine ili kuharakisha juhudi zake za uchapishaji wa vitabu.
Wakati huo huo, Profesa Said alimweleza  Bwana Yussuf kuwa hadi sasa ameshaandika vitabu takribani 57 na moja ya kati ya kitabu chake kinachotamba kwa sasa ni riwaya yake  inayokwenda kwa jina la ‘Kamwe Si Mbali Tena’ ambacho pia alimkabidhi Bwana Yussuf Shoka nakala ya kitabu hicho.
Katika mazungumzo yao, Profesa aligusia nukta mbali mbali zinazohusiana na Elimu na maendeleo ya taifa pia sambamba nay ale ya uandishi wa vitabu na kupanuka kwa kiwango cha taaluma nchini.
‘Jamii ya Watanzania kwa sasa imepanuka kifikra na kimawazo. Ninaposema hivi sikusudii wasomi tu, bali hata Watanzania wasiosoma wametanuka sana kiupeo kiasi ambacho kasi ya maendeleo nchini inakuwa kubwa. Hivyo, ni busara kabisa kwa wasomi kurejea nchini na kushirikiana na wenzao wengine katika kuharakisha maendeleo hayo!’ Alisema Profesa Said.

Profesa Said ni mwalimu mstaafu kwa sasa aliyeamua kwa makusudi kurejea nchini kujiunga na wazalendo wengine katika kusukuma mbele maendeleo ya Taifa ambapo kwa sasa na kwa nyakati tafauti amekuwa akifundisha katika chuo kikuu cha Taifa (SUZA) na chuo kikuu kishiriki cha Elimu Chukwani.

Naye Bwana Yussuf Shoka ambaye  ni mzaliwa wa Wingwi, Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba ni mhadhiri wa Kiswahili na Fasihi katika chuo kikuu cha London (SOAS) na pia anafundisha Kiswahili katika chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza.

No comments: