Monday, August 31, 2015

STARTIMES YAZINDUA KIPINDI CHA TELEVISHENI MASHARIKI MAX

 Makamu Rais wa kampuni ya StarTimes, Bw. Michael Dearham (kushoto) akisalimiana na Jokate Mwegelo (kulia) atakae kuwa mtangazaji wa kipindi cha Mashariki Max kitakacho onyeshwa na StarTimes kupitia chaneli ya ST Swahili, wakati wa uzinduzi wa kipindi hicho uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Katikati ni mtangazaji wa kipindi hicho nchini Kenya, Sarah Hassan. Picha na mpiga picha wetu. 
 Makamu Rais wa kampuni ya StarTimes, Bw. Michael Dearham (kushoto) akiwapungia mkono wageni pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes, Bw. Lanfang Liao (kulia) wakati wa uzinduzi wa kipindi cha Mashariki Max kitakacho onyeshwa na StarTimes kupitia chaneli ya ST Swahili. Uzinduzi huo uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Picha na mpiga picha wetu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes, Bw. Lanfang Liao (katikati) katika picha ya pamoja na watangazaji wa kipindi cha Mashariki Max Jokate Mwegelo (kulia) na Sarah Hassan (kushoto) wakati wa uzinduzi wa kipindi cha Mashariki Max kitakachoonyeshwa na StarTimes kupitia chaneli ya ST Swahili. Uzinduzi huo uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Picha na mpiga picha wetu. 

Na Mwandishi Wetu
STARTIMES  Tanzania kupitia chaneli yake mahususi ya vipindi vya kishwahili, StarTimes Swahili imezindua kipindi cha Mashariki Max ambacho kitakuwa kinaangazia mitindo na maisha ya watu mbalimbali maarufu nchini.

Kipindi hicho kilichozinduliwa jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Serena mwishoni mwa wiki kitakuwa kikitangazwa na mrembo Jokate Mwegelo ambaye licha ya kuwa alishawahi kuwa mshindi wa pili wa shindano la Miss Tanzania, pia ni mwanamuziki, mcheza filamu na pia mjasiriamali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mgeni rasmi ambaye ni Makamu wa Rais wa StarTimes Africa, Bw. Michael Dearham amesema kuwa, “Tunayo furaha siku ya leo kuzindua kipindi cha Mashariki Max kwani kitaongeza uhondo wa vipindi veytu vya kuvutia tulivyonavyo,Kuongezewa kwa kipindi hiki katika chaneli ya StarTimes Swahili kuna maana kubwa katika kujenga, kukuza na kuithamini lugha ya Kiswahili ambayo inatumika sehemu kubwa ya Afrika Mashariki na Kati.”

Bw. Dearham aliendelea kwa kusema, “Kipindi hiki cha Msahriki Max kitaanza kuruka siku ya Jumamosi ya Septemba 5 kuanzia saa 12:30 jioni na kila, tunaamini kuwa kwa kuzidi kuongeza vipindi ambavyo vina maudhui mengi ya Kiswahili wateja wetu wataburudika. Kipindi hiki tunaamini kuwa hakitaonekana ukanda wa Afrika ya Mashariki au Afrika nzima bali hata sehemu zingine za dunia.”

Aliongezea kuwa licha ya StarTimes kuwekeza nguvu katika kuongeza na kuboresha vipindi vya nyumbani pia inajitahidi kadiri ya uwezo wake kuongeza zaidi chaneli na vipindi vya michezo nchini hususani vya mpira wa miguu.

“Mbali na kuongeza na kuboresha vipindi vyenye maudhui ya nyumbani pia tunafuta fursa za kuboresha vipindi na chaneli za michezo, tuna mipango ya kuboresha na kukuza michezo nchini kama vile kudhamini mashindano na timu za soka nchini ili kuinua sekta hii,” alisema na kuongezea Bw. Dearham kuwa, “Licha ya vipindi vingine sasa hivi wateja wetu wanayo fursa ya kufurahia ligi mbalimbali bora za mpira wa miguu duniani kama vile ya Ujerumani (Bundesliga) na  Italia (Serie A) ambazo zipo mahususi kupitia visimbuzi vyetu vya StarTimes.”

“Tunayo furaha sana kuona watejea wetu wanafurahia vipindi vyite hivi ambavyo tunazidi kuvitambulisha kwenu kila kukicha, napenda kuwaambia kuwa StarTimes itazidi kuwaletea huduma na bidhaa nzuri na vipindi bor ana vya kusisimua zaidi.” Alihitimisha bosi huyo wa StarTimes

Naye kwa upande wake mtangazaji wa kipindi hicho mrembo Jokate Mwegelo alibainisha kuwa kwake hii ni heshima na fursa kubwa sana kwake kwani StarTimes imesambaza huduma zake sehemu kubwa ya bara la Afrika.

“Nimekwisha tangaza vipindi mbalimbali vya luninga lakini hiki cha Mashariki Max kupitia chaneli ya StarTimes Swahili kitanipa fursa kubwa ya kukua kwani nitakuwa nikionekana sehemu kubwa ya Afrika ya Mashariki na Afrika nzima kwa ujumla.”

Aliongezea kwa kusema kuwa wateja wote wa StarTimes wakae mkao wa kula na kutegemea mambo mazuri kwani kipindi hiki kitakuwa na maudhui bomba yanayohusu mitindo, maisha ya watu maarufu wa tasnia mbalimbali pamoja na tamaduni kwa ujumla.

“Ninategemea watazamaji licha ya kuburudika kupitia kipindi cha Mashariki Max pia wataweza kujifunza na kujua mambo mbalimbali watu wanayopitia mpaka kufanikiwa katika maisha yao. Nina hakika hii ni fursa kwa kujifunza kupitia simulizi tamu za maisha ya watu wengine.” Alihitimisha mrembo huyo.

No comments: