Sunday, August 28, 2016

JAFO AFANYA ZIARA YA SIKU MBILI MKOA WA SHINYANGA NA GEITA


Naibu waziri Ofisi ya rais, Tamisemi, Selemani Jafo, akizungumza na wananchi nje ya kiwanda cha kukamulia alizeti mjini Chato.
Naibu waziri Ofisi ya rais, Tamisemi, Selemani Jafo, akikagua mashine za kukamulia mafuta ya alizeti mjini Chato.
Mkurugenzi wa mji wa Kahama, Andason Msumba akitoa maelezo kwa Naibu waziri Ofisi ya rais, Tamisemi, Selemani Jafo kuhusu mgogoro wa soko  wanalolitaka wananchi kutumika kwa maslahi ya wananchi wa mji huo. 
Naibu waziri Ofisi ya rais, Tamisemi, Selemani Jafo, akikagua mradi wa maji  kijiji cha Chankorongo wilayani Geita uliohujumiwa na watendaji na kumuagiza Katibu tawala wa mkoa wa Geita kuunda timu ya uchunguzi.

Naibu waziri Ofisi ya rais, Tamisemi, Selemani Jafo, akiwa katika harambe ya kuchangia madawati mkoani Geita, kulia kwake ni Mkuu wa mkoa huo Meja jenerali mstaafu Ezekiel Kiunga pamoja na Mwenyekiti wa harambee hiyo, Ignas Inyasi.
Naibu waziri Ofisi ya rais, Tamisemi, Selemani Jafo, akizungumza katika harambe ya kuchangia madawati mkoani Geita, ambayo alikuwa akimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo amefanya ziara ya Siku mbili katika mikoa ya Shinyanga na Geita na kukagua miradi mbalimbali.

Akiwa Mkoani Shinyanga, Jafo alitembelea Hospitali ya Wilaya ya Kahama ambapo alijionea changamoto mbali mbali ikiwepo ya Jengo dogo linalotumiwa na kinamama wakati wakujifungua kutokana na hospitali hiyo kuzidiwa uwezo.

Kufuatia hali hiyo, Jafo amemuagiza Injinia wa Wilaya kuhakikisha wanaharakisha ujenzi wa Jengo kubwa la kisasa la kinamama kwani fedha zipo za Ujenzi huo ili wagonjwa wasiendelee kupata mateso kwa michakato ya Ujenzi mirefu isiyo na tija.

Kadhalika, akiwa wilayani Kahama, Naibu Waziri Jafo ametembelea Mradi wa Soko na kumuagiza Mkurugenzi wa Wilaya, Andason Msumba, kuhakikisha anakaa na timu yake ya Wataalamu ili kutatua mgogoro wa Soko hilo kwa Maslahi mapana ya wananchi wa Mji wa Kahama.

Amehitimisha Ziara yake mkoani Shinyanga kwa kuzungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama na Halmashauri ya Msalala ambapo amewataka Watumishi kufanya kazi kwa kujituma huku wakiepuka Uzembe kazini,upendeleo, kupigana majungu, na kuchukiana.

Katika mkoa wa Geita, Jafo amekagua mradi wa Maji na Kiwanda cha kukamua mafuta ya Alizeti wilayani Chato huku akimuagiza Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo kuhakikisha mradi unakamilika mapema kabla ya Mwezi wa 10 ili kuweza kusaidia kutatua changamoto ya Maji.

Amesema wananchi hawawezi kuwa na Upungufu wa Maji wakati kuna maji mengi ya Ziwa Victoria. Akikagua Mradi wa kiwanda cha kukamua Mafuta ya Alizeti, Jafo alimwagiza Mkurugenzi kuhakikisha anashirikiana na Sido ili kuweza kuukamilisha mradi huo haraka.

Akiwa njiani kuelekea Geita mjini, Jafo alipita Jimbo la Busanda wilaya ya Geita Vijijini na Kukagua Mradi wa Maji uliokamilika Kijijini Makondeko kisha Safari ikaelekea Kijiji cha Chankorongo ambapo kuna Mradi wa Maji wa muda mrefu usio kamilika ambapo mpaka sasa umetumia zaidi ya Bilioni moja na dalili za kukamilika bado.

Kufuatia hali hiyo, Naibu Waziri huyo amemwagiza Katibu tawala wa Mkoa wa Geita Selestine Gesimba kuunda tume maalum ya kuchunguza sakata la mradi huo wa maji wa Chankorongo ambapo wamepewa mwezi mmoja kukamilisha uchunguzi huo.

Alimwagiza Katibu Tawala Mkoa akishirikiana na Wakurugenzi wote kuhakikisha suara la Oprass linapewa kipaumbele kwa watumishi na linafanyika kwa wakati na ipasavyo. Naibu Waziri aliwahakikishia watumishi kuwa serikali inafuatilia changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuwataka wawe na Subra.


Wakati huo huo, akiwa Mkoani Geita Jafo alimwakilisha Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa katika Harambee ya ya kuchangia Madawati.

Katika harambe hiyo Jafo alihamasisha na kuweza kukusanywa kiasi cha Shilingi Bilioni Moja, mia saba arobaini Milioni , laki tano na elfu tisini na saba (1,740,597,000) Kiasi ambacho kilimfanya Mkuu wa Mkoa huo Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga kumshukuru sana Naibu waziri huyo kwani  hakutegemea kiasi hicho kikubwa cha Fedha kuweza kupatikana. 

No comments: