Sunday, December 4, 2016

WAZIRI MKUU AAGIZA UCHUNGUZI UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA MONDULI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo kufanya uchunguzi na kumpelekea taarifa ya watendaji waliohusika katika ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa mradi wa hospitali ya wilaya ya Monduli uliogharimu sh. bilioni 2.7.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Desemba 4, 2016) wakati akizindua hospitali ya wilaya ya Monduli ambayo katika ujenzi wake kulitakiwa kuwe na jengo la maabara ambalo halipo na fedha zimeisha.
"Mkuu wa Mkoa shirikiana na Sekretarieti yako kufanya uchunguzi na atakayebainika kuhusika kwenye ubadhirifu huu achukuliwe hatua za kisheria kwa sababu ujenzi huu ulihusisha na jengo la maabara lakini tayari mradi umekamilika na hakuna jengo la maabara," amesema.
Naye Mkuu wa mkoa huo Bw. Gambo amesema tayari wameanza kufanya uchunguzi wa ujenzi wa mradi huo baada ya kubaini kuwa umetumia kiasi cha fedha kilichotumika hakilingani na thamani ya mradi huo.
Mkuu huyo wa Mkoa ameahidi kufuatilia suala hilo na uchunguzi utakapokamilika taarifa hiyo itapelekwa kwa Waziri Mkuu.
Awali, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Zaveri Benela akisoma taarifa ya hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya jengo la upasuaji karibu na wodi ya wazazi hali inayowalazimu kuwasafirisha wagonjwa umbali wa zaidi ya mita 300 hadi kwenye jengo la upasuaji lililopo katika majengo ya zamani.
Pia kukosekana kwa jengo la wagonjwa wa nje na jengo la maabara kwenye majengo hayo mapya hali inayochangia huduma kutolewa kwenye maeneo miwili tofauti kwa wakati mmoja yaani katika wodi mpya na majengo ya zamani na hali hivyo inaleta usumbufu kwa wagonjwa.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu  ametoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Bw. Idd Kimanta kumaliza tatizo la  mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Emairete kilichopo Monduli juu mkoni hapa  baada ya kudumu kwa miaka 20.
Mgogoro huo ni wa shamba kubwa ambalo awali lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya bia ya Breweries na kisha  kurejeshwa kwa kijiji hicho ambapo viongozi wa viongozi wa zamani wa  Kijiji hicho walijimilikisha kinyemela.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kusimamishwa na wanakijiji hao waliokuwa  wamebeba mabango ya kumuomba  msaada wa kutatuliwa kwa mgogoro huo wakati anatoka kudhuru kaburi la Waziri Mkuu wa zamani Hayati Moringe  Sokoine.
Waziri Mkuu alimtaka mkuu huyo wa wilaya kueleza sababu za kwa ya nini uongozi wa wilaya umeshindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  William Lukuvi ambaye alifika kijijini hapo na kutoa maelekezo.
Baada ya maelekezo hayo Waziri Mkuu aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa na imani ya Serikali ya awamu ya tano  inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli ambayo ipo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hasa wanyonge.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo amekiri kuwepo kwa mgogoro huo kwa miaka 20 na kwamba Waziri Lukuvi alitoa maelekezo ambayo halmshauri inayafanyia kazi na imeshindwa kuleta majibu kwa wananchi hao kutokana na ziara ya Waziri Mkuu ambaye aliwataka watekeleze majukumu yao na wasitumie ziara yake kama kisingizio.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Serikali na Watanzania wote wanatambua  na kuiheshimu kazi nzuri iliyofanywa na hayati Sokoine kwa Taifa kipindi cha uhai wake na itaendelea kuienzi. Pia  Serikali itaendelea kushirikiana na familia katika mambo mbalimbali.
Wakati huo huo, WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti  kubadilisha uongozi wa  Kituo cha afya cha Levolosi baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa kinatoa huduma mbovu kwa wagonjwa hususan ni kwa wajawazito.
Pia amewataka wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kujenga hospitali za wilaya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za rufaa.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Desemba 4, 2016)  wakati alipotembelea  Hospitali ya mkoa ya Mount  Meru, ambapo alisema 
tatizo la msongamano wa wagonjwa hospitali za rufaa na hospitali nyingine ni lazima lipatiwe ufunguzi.

"Hatuhitaji kuwa na madaktari ambao wanasumbua wagonjwa. Daktari wa Mkoa hakikisha kile kinacholalamikiwa kule Levolosi kinatafutiwa ufumbuzi. Hapa Mount Meru hakikisheni mnaboresha mazingira ya vyoo kwenye wadi  za wazazi pamoja na kujenga sehemu ya kuoshea vyombo kwa wagonjwa, " alisema.
Awali alipotembelea wodi ya kinamama wanaosubiri kujifungua, mmoja wa wagonjwa, Glory Paul Mkazi wa Olasiti alimweleza Waziri Mkuu kuwa mtoto wake alifia tumboni baada ya wauguzi na  madaktari wa kituo cha Afya cha Levolosi  kuchelewa kumpatia matibabu.
"Wakati nahudhuria kliniki nishaambiwa na daktari kuwa natakiwa kujifungua kwa njia ya upasuaji na siwezi kujifungua kwa njia ya kawaida nilimwambia nesi kuwa  natakiwa kufanyiwa upasuaji wakanikatalia na kunilazimisha nijifungue kwa njia ya kawaida ambapo ilishindikana na baada ya muda waliniambia kuwa mtoto amekufa na wananifanyia upasuaji ili kuokoa maisha yangu," amesema..

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia alisema amepokea maagizo ya Waziri Mkuu, ambayo yanalenga kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza kuwa awali alichukua hatua za kinidhamu kwa watoa huduma za afya kituoni hapo na ataendelea kusimamia nidhamu ya kazi ili kuondoa malalamiko kwa wananchi juu ya huduma za afya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, DESEMBA 4, 2016.

No comments: