Wednesday, April 26, 2017

MAGAZETI YA LEO JUMATANO APRIL 26,2017


SERIKALI YAWATAKA WAAJIRI KUHAKIKISHA MITAMBO NA VIFAA VYA KAZI VINAFANYIWA UKAGUZI MARA KWA MARA.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde akitoa hotuba yake wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi uliofanyika Aprili 25, 2017 Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) wakimsikiliza Naibu wake Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Antony Mavunde (hayupo pichani) wakati wa Mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi hiyo ikiwa ni maandalizi ya ya maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi uliofanyika Mjini Dodoma.
Kaimu Mtendaji Mkuu OSHA Bi. Khadija Mwenda akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa habari juu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya mahali pa Kazi uliofanyika Mjini Dodoma Aprili 25, 2017.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw.Peter Kalonga akichangia hoja wakati wa Mkutano na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya mahali pa Kazi uliofanyika Mjini Dodoma Aprili 25, 2017.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde akisalimiana na Mwakilishi wa TUCTA Bw.Ramadhani Mwenda mara baada ya mkutano wa waandishi wa habari Aprili, 25, 2017 Dodoma
Naibu wake Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA)mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari Aprili 25, 2017 Mjini Dodoma. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU-DODOMA)

………….

Na. Mwandishi Wetu- Dodoma


Serikali imewataka waajiri wote na wadau kwa ujumla kuhakikisha kuwa sehemu za kazi, mitambo na vifaa vya kufanyia kazi vinafanyiwa ukaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa havileti madhara kwa wafanyakazi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Ajira na Vijana Mhe. Antony Mavunde wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi.

“Kwa upande wa Serikali jukumu letu kubwa ni kuweka na kusimamia sera ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kutunga na kusimamia Sheria za Usalama na Afya Mahali pa Kazi, na kuweka viwango mbalimbali vya usalama na afya sehemu za kazi” alisisitiza Mavunde.

Mavunde alisema kuwa kwa sasa kanuni ya kuripoti ajali na magonjwa imekamilika na kuanza kutumika tangu mwezi Septemba, mwaka 2016.

Ambapo ameshauri wafanyakazi kuwasaidia waajiri wao kusimamia mifumo iliyopo, kujilinda wao binafsi ili wasiumie ama wasipate magonjwa yatokanayo na kazi sambamba na kutumia ipasavyo vifaa vyote vya kujikinga wawapo kazini.

Mavunde alisema kuwa serikali inaendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji takwimu za ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, hivyo bado kuna changamoto ya kupata taarifa kuhusu ajali na magonjwa yatokanayo na kazi hii inatokana na waajiri wengi kutoripoti taarifa hizo kama sheria inavyoelekeza.

kwa mantiki hiyo Serikali inaandaa mfumo ambao utaongea na mifumo mingine ili kupata taarifa za ajali na magonjwa.

Aliongeza kuwa “Serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) imejipanga kuhakikisha kuwa Usalama na afya za wafanyakazi hao zinalindwa kwa kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia taratibu zote za Usalama na Afya kwa mujibu wa sheria na 5 ya Mwaka 2003, ili kulinda nguvu kazi ya taifa hili”.

Aidha, tarehe 28 Aprili ya kila mwaka, Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Usalama na Afya Mahali pa kazi ili kuwakumbuka wahanga wa majanga yanayotokea sehemu za kazi.

Madhumuni makubwa ya kuadhimisha siku hii ni kuendesha kampeni ya Kimataifa ya kuboresha usalama na afya kazini na kuhamasisha utengenezaji ajira zenye staha. Kwa kuhamasisha waajiri na wafanyakazi na umma kwa ujumla kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha kuwa suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi yanapungua au kutotokea kabisa sehemu za kazi.

Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajia kufanyika Moshi Mkoani Kilimanjaro kwa kujumuisha shughuli hizo kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 ambapo yatatanguliwa na kongamano la wadau wa Usalama na Afya.

ZANZIBAR YAJIANDAA KUMALIZA KABISA MALARIA 2023

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt, Fadhil Mohd Abdalla akimkaribisha Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman kuzungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi. Harusi Said Suleiman akizunguza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Mwandishi wa habari wa ITV/Radio One Farouk Karim akiuliza swali katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa mkutano wa waandishi wa habari katika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Meneja Kitengo cha Kumaliza Malaria Zanzibar Mwinyi Issa Khamis akijibu maswali ya waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya malaria yaliyoadhimishwa kwa mkutano wa waandishi wa habari Wizara ya Afya Zanzibar .Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar

Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman amesema pamoja na mafanikio makubwa katika kupambana na Malari Zanzibar, bado shehia tano zinaendelea kutoa wagonjwa wa maradhi hayo zaidi ya asilimia tano.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano wa Wizara ya Afya Mnazimmoja, amezitaja shehia hizo kuwa ni Tumbatu Jongowe, Miwani, Micheweni, Chukwani na Kiwengwa.

Hata hivyo amesema maambukizi ya malaria katika maeneo hayo yanasababishwa na wasafiri wanaoingia na kutoaka nje ya Zanzibar mara kwa mara ambapo mwaka jana asilimia 55 ya wagonjwa waliogundulika walikuwa na tabia hiyo.

Amesema takwimu za Malaria Zanzibar zinaonyesha mafanikio mazuri ambapo mtu mmoja kati ya watu mia moja hupata ugonjwa huo katika jamii isipokuwa shehia hizo tano.

Naibu Waziri wa Afya amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na Malaria ikiwemo kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa na kusafisha mazingira kwa lengo la kuondosha mazalio ya mbu wanaoeneza maradhi hayo.

Ameongeza kuwa Serikali kwa upande wake mwaka jana iligawa vyandarua 705,000 bila malipo na kufanya zoezi la kupiga dawa nyumba za wananchi ya kukinga malaria bila ya kuangalia vyeo vya wamiliki wa nyumba hizo licha ya kukabiliana na changamo nyingi katika kazi hiyo.

Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikataa kupigiwa dawa nyumba zao kwa madai kwamba zinawaletea athari za afya jambo ambalo halina ukweli kwani dawa hiyo ni salama kwa afya.

Amekubusha kuwa Sheria ya Afya ya Jamii na Mazingira ya mwaka 2012 pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya udhibiti wa mbu na mazingira hivyo wananchi watakaokataa kupigiwa dawa sheria itawabana.

“Watu wanaokataa nyumba zao kupigiwa dawa ya kukinga maluaria bila sababu za msingi zinazokubalika, sheria hii itawabana na hatua muafaka zitachukuliwa dhidi yao, ” alisisitiza Naibu Waziri.

Meneaja Kitengo cha kumaliza malaria Mwinyi Khamis alisema Zanzibar imeweka mikakati ya kumaliza kabisa malaria ifikapo mwaka 2023 hivyo juhudi za jamii na Wizara ya Afya ni muhimu.

Amesema mwaka jana watu watano walibainika kufa kwa malaria Zanzibar wakiwemo watoto wawili wenye umri chini ya miaka mitano.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Mohd amewashauri wananchi wasikubali kula dawa ya malaraia bila kupimwa na kuthibitishwa kuwa wanayo malaria.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasema Malaria bado ipo Zanzibar, chukua tahadhari.

Tuesday, April 25, 2017

SIMBA YAIFUATA DAWA YA KUIA AZAM JUMAMOSI KOMBE LA FA

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

KIKOSI cha timu ya Simba kimeendelea kujifua kwa nguvu wakijiandaa na mchezo wa nusu fainali dhidi ya Azam utakaofanyika mwishioni mwa wiki hii.

Jumamosi ya April 29, ni nusu fainali ya kwanza ya kombe la Shirikisho la Azam HD baina ya Simba na Azam itakaopigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa.

Kwa sasa Simba wapo Morogoro wakijiandaa na mchezo huo ambapo chini ya Kocha Joseph Omog na Jackson Mayanja kimeamua kujichimbia huko kwa ajili ya kuwapa muda wa kupumzika wachezaji wake na kuwapa mbinu mpya mbalimbali.

Hii inakuwa ni mechi ya ushindani mkubwa sana kwa timu hizi mbili zikikutana kwa mara ya tatu ndani ya msimu mmoja ambapo katika michezo miwili ya awali ila mmoja akishinda mchezo mmoja.

Kwa mujibu wa Kiongozi wa Simba, Abbas Ally amesema kuwa wachezaji wana ari kubwa sana na wako vizuri na wanaamini watapigana mpaka mwisho ili kupata ushindi kwenye mchezo huo.

"Huu ni mchezo muhimu sana kwetu, ni muhimu kupata ushindi  ili tuweze kuingia fainali ya kombe la Shirikisho na wachezaji wana ari kubwa sana ya ushindi na wameahidi kupambana mpaka mwisho,"amesema Ally.

Mpaka sasa Kikosi cha Simba kinakabiliwa na majeruhi wawili ambao wanatarajiwa kuukosa mcheoz huo ambao ni Hamad Juma na Jamal Mnyate.
Wachezaji wa Simba wakiwa katika mazoezi ya pamoja kulekekea mchezo wao wa nusu fainali ya kombe la Shirikisho la Azam HD siku ya Jumamosi dhidi ya Azam. Golikipa Peter Manyika akiwa katika mazoezi  kulekekea mchezo wao wa nusu fainali ya kombe la Shirikisho la Azam HD siku ya Jumamosi dhidi ya Azam.
 
 Wachezaji wa Simba wakimsikiliza Kocha Joseph Omog katika maandalizi ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam HD siku ya Jumamosi.
Wachezaji wa Simba wakiwa katika mazoezi ya pamoja kulekekea mchezo wao wa nusu fainali ya kombe la Shirikisho la Azam HD siku ya Jumamosi dhidi ya Azam.

MAHAKAMA KUU TANGA YAJIPANGA KUMALIZA KESI

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga
Mhe. Imani Abood Muonekano wa majengo ya Mahakama Kuu
kanda ya Tanga baada ya kukamilika kwa ukarabati
Na Lydia Churi- Mahakama

Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16-2019/2020) pamoja na Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama, imepania kuhakikisha kuwa kesi zote za zamani pamoja na zile zinazosajiliwa zinamalizika ili wananchi waweze kuwa na kujenga imani zaidi na chombo hicho muhimu cha utoaji wa haki nchini. Katika kulitekeleza hili, ipo mikakati iliyowekwa na Mahakama kwa ujumla na ile inayowekwa na kila Kanda ya Mahakama Kuu nchini.

Mikakati ya Mahakama ni pamoja na Majaji na Mahakimu kupangiwa idadi ya kesi watakazotakiwa kuzisikiliza na kuzimaliza katika kipindi cha mwaka mmoja. Kila Jaji amepangiwa kumaliza kesi 220 kwa mwaka na kila hakimu anatakiwa kusikiliza kesi 250 kwa mwaka. Mkakati mwingine wa jumla ni kiwango cha muda kilichopangwa kwa kesi kukaa Mahakamani, mathalani, Mahakama ya Tanzania imepanga kuwa kesi zote zilizosajiliwa Mahakama Kuu zisikae Mahakama kwa muda unaozidi miaka miwili wakati katika Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na zile za wilaya imeamuliwa kesi isizidi miezi 12 Mahakamani. Kesi katika Mahakama za Mwanzo inatakiwa kumalizika katika kipindi cha miezi sita.

Aidha, Mahakama imeanzisha utaratibu wa kufanya vikao na wadau wake ili kujadili namna ya kumaliza kesi kwa wakati kama moja ya mikakati yake ya kuhakikisha kesi zote za zamani zinamalizika Mahakama na pia kesi zinazosajiliwa zinamalizika kwa wakati ili kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuwapatia wananchi wa Tanzania Haki sawa na kwa wakati.

Pamoja na kuwepo kwa mikakati ya Mahakama ya kumaliza kesi zilizoko Mahakamani, Mahakama Kuu kanda ya Tanga nayo imejiwekea mikakati yake ili kuhakikisha inaenda sambamba na kasi ya Mhimili huo ya  kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati kwa kumaliza kesi zao kwa wakati.

Akizungumzia suala la kumalizika kwa kesi kwa wakati, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga Mheshimiwa Imani Abood alisema kanda yake imepanga kuwanunulia Mahakimu wake wote (68) kompyuta Mpakato (Laptops) zitakazowasaidia katika kurahisisha kazi zao na kuondosha mashauri kwa wakati katika Mahakama mbambali za mkoa wa Tanga. Alisema lengo ni kuhakikisha Mlundikano wa kesi zilizopo Mahakamani unaisha na pia kesi zinazosajiliwa zinamalizika kwa wakati.

Jaji Mfawidhi alifafanua kuwa kompyuta hizo zitawasaidia waheshimiwa Mahakimu katika kuandika hukumu ili wananchi waweze kupati haki kwa wakati. Aliongeza kuwa hivi sasa Mahakimu wa mahakama za Mwanzo huandika hukumu kwa kalamu na baadaye hukumu hizo hupelekwa kwenye mahakama za wilaya ambapo kuna umeme kwa ajili ya kuchapwa na baadaye hurudishwa kwenye kwenye Mahakama za Mwanzo.

Alisema pia kanda yake inakabiliwa na uhaba wa watumishi hasa Makatibu Muhtasi pamoja na vitendea kazi jambo ambalo limekuwa likichelewesha utolewaji wa hukumu pamoja na upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati. Aliongeza kuwa kwa Mahakimu kupatiwa kompyuta hizo kutarahisisha upatikanaji wa haki.
Pamoja na kuwapatia Mahakimu Kompyuta, Jaji Abood alisema Mahakama Kuu Kanda ya Tanga inao mpango wa kuhakikisha inazipatia umeme baadhi ya Mahakama za Mwanzo kupitia Mradi wa Umeme vijijini (REA) ili kurahisisha upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati. Na hivi sasa tayari Mahakama za Mwanzo tano zimeshapatiwa umeme.


Jaji Abood aliitaja mipango mingine iliyowekwa na Kanda yake katika kuitekeleza nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania ya kuwapatia wananchi haki kwa wakati kuwa ni kuwapeleka Mahakimu wenye kesi chache kwenye Mahakama zenye kesi nyingi na upungufu wa Mahakimu ili kuhakikisha mashauri yote ya muda mrefu yanaondoshwa na yaliyofunguliwa yanamalizika kwa wakati.

Aliitaja mikakati mingine waliyojiwekea ili kuondosha mlundikano wa kesi Mahakamani kuwa ni pamoja na Majaji na Mahakimu kugawana idadi sawa ya Mashauri yaliyopo Mahakamani, kutenga vipindi maalum vya kumaliza kesi zote, Mahakimu wenyewe kufanya kazi ya kuchapa hukumu ili kesi zimalizike kwa wakati na kufanya vikao na wadau ili kuweka mikakati ya kumaliza kesi kwa wakati.

Kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania kwenye kanda ya Tanga, Jaji Mfawidhi alisema kuwa utekelezaji wa Mpango huo unaendelea vizuri baada ya kuwa wamejiwekea mikakati ya utekelezaji. Alisema hivi sasa kuna mageuzi makubwa kwenye Mahakama za Mwanzo hasa zile zenye umeme. Nakala za hukumu zinapatikana kwa wakati (ndani ya siku 21) na, mienendo ya kesi ndani ya siku 90 ikiwa ni pamoja na kesi kumalizika kwa wakati.  

Kuhusu maendeleo ya Mradi wa kupambana na Rushwa ndani ya Mahakama (STACA), Jaji Mfawidhi anasema Mradi huu wa Mahakama ya Tanzania umeleta mageuzi makubwa ndani ya Mahakama hasa Kanda ya Tanga kupitia vifaa vilivyosambazwa (pikipiki, baiskeli mabango na simu).

Alisema kuwa suala la mapambano dhidi ya Rushwa ndani ya Mahakama linatiliwa mkazo na Mahakama Kuu kanda ya Tanga. Watumishi wa kanda hii wamekuwa wakikumbushwa mara kwa mara juu ya kufuata maadili katika kazi zao na kuepukana na vitendo vya rushwa. Alisema kufuatia mabango yaliyosambazwa na Mahakama katika Mahakama za Mwanzo zote, Mahakama za wilaya, mahakama ya |Mkoa, mahakama kuu, ofisi za halmashauri na ofisi za wakuu wa wilaya, jamii imeanza kubadilika kimtazamo kuhusu Mahakama akisema hivi sasa malalamiko yamepungua kwa kiasi kikubwa katika kanda yake.

Taarifa ya malalamiko  ya mwezi Februari 2017 inaonyesha kulikuwa na malalamiko 3 tu kwa kanda nzima ikilinganishwa na malalamiko 11 yaliyokuwepo kipindi cha mwezi Januari, 2017 na malalamiko 15 katika kipindi cha mwezi Septemba, 2016. Kusambazwa kwa vifaa kama vile Pikipiki na Baiskeli kumesaidia Mahakamu kuweza kutembelea Mahakama za Mwanzo zenye idadi kubwa ya kesi na kuzimaliza hivyo kusaidia kumaliza mlundikano wa kesi.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Afisa Utumishi wa Kanda hiyo, Farid Mnyamike alisema hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Magoma iliyoko Korogwe pamoja na ukarabati wa jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Old Korogwe. Alisema kazi hiyo inafanywa na mkandarasi, SUMA JKT ambaye kwa sasa amefikia zaidi ya asilimia 70 ili kukamilisha kazi hiyo. Mkandarasi alikabidhiwa kazi hiyo Februari 2, 2017 na  anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu alipokabidhiwa. Aidha, Mradi wa Ukarabati wa majengo ya Mahakama Kuu tayari umekamilika na majengo yalishakabidhiwa kwa Mahakama ya Tanzania.

Mahakama kuu kanda ya Tanga pamoja na kanda nyingine zinakabiliwa na tatizo kubwa la kuwa na miundombinu mibovu hasa kwa upande wa majengo ya Mahakama nyingi za Mwanzo. Mahakama Kuu kanda ya Tanga inayo majengo 68 ya Mahakama ambapo Mahakama 30 ndizo zinazofanya kazi wakati 12 ni zile zinazotembelwa na Mahakama 26 hazifanyi kazi kabisa.

Katika kutatua tatizo la ukosefu na uchakavu wa majengo ya Mahakama nchini, Mahakama ya Tanzania inatarajia kukamilisha miradi ya ukarabati na ujenzi wa majengo 70 ya Mahakama katika kipindi cha miaka miwili ili kusogeza karibu huduma ya utoaji haki kwa wananchi. Majengo tisa ya Mahakama kuu yanatarajiwa kujengwa na kukamilika katika mikoa tisa ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya siku ya Sheria nchini, Kaimu jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma alisema Mahakama sita za Mikoa zitajengwa ndani ya miezi 6-12 wakati Mahakama za Wilaya 19 na za Mwanzo 36 zinatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2017.